Text Size

Tamko la Viongozi wa Makanisa

Tamko la Viongozi wa Makanisa
Barasa la Maaskofu Katoliki Tanzania - Tec Na Jumuiya ya Kikristo Tanzania - CCT
Septemba 2004

1.1 Uchaguzi wa Viongozi
Tanzania itakuwa na uchaguzi wa viongozi wa Vitongoji, Mitaa na Vijiji mwaka huu wa 2004 na uchaguzi wa Madiwani, Wabunge na Rais mwaka 2005. Uchaguzi wa mara kwa mara ni njia bora ya kidemokrasia ya kuwapata viongozi. Kupiga kura na kugombea uongozi ni jambo linalopendeza na kukubalika mbele ya Mwenyezi Mungu. Ni wajibu na haki kwa raja wote nchini kushiriki kikamilifu katika kupanga, kuweka na kuendesha utawala wa Taifa lao.
Watanzania tumejijengea utamaduni wa kujiandikisha na kuwapigia kura viongozi wanaofaa kuiongoza nchi yetu. Baada ya kuonja matunda ya demokrasia ya vyama vingi kwa miaka hii 12, inabidi tuwe tumekomaa na wazoefu zaidi katika kutumia haki zetu za msingi kuwachagua viongozi wanaotufaa.
Sisi Viongozi wa CCT na TEC tunachukua nafasi hii kuwahimiza Watanzania kuwa na uchaguzi huru, wa haki na amani ili kuwapata viongozi bora ambao watatanguliza maslahi ya Taifa kuliko ya kwao binafsi. Tunalo jukumu la pamoja la kufanikisha Uchaguzi wa 2004 na Uchaguzi Mkuu wa 2005. Yafuatayo ni mapendekezo yetu na maelekezo yetu ya msingi kwa Watanzania wote katika kufanikisha azma hii.
1.2 Viashiria vya Kuvunja Amani
Kwanza tunamshukuru Mungu kwa jitihada za Serikali yetu katika kukuza demokrasia na kutunza tunu ya amani katika chaguzi zilizopita. Hata hivyo, uzoefu unaotokana na chaguzi zilizopita umeonyesha kuwa katika baadhi ya chaguzi kumekuwa na manung'uniko juu ya matumizi ya rushwa yanayosababisha kupata baadhi ya viongozi wasio waadilifu. Aidha kumekuwa na viashiria vya kuvunja amani na dalili za unyanyasaji unaofanywa wakati mwingine na baadhi ya viongozi wa vyama mbali mbali vya siasa.
Vile vile utamaduni wa kidemokrasia wa kutofautiana na/au kupingana bila kupigana na wa kuheshimu uhuru wa mtu kutoa mawazo yake, umekuwa ukikosekana kwa baadhi ya viongozi wa siasa na wanachama wao. Wakati mwingine uvumilivu wa kisiasa na hata wa kidini ni tunu iliyoonekana kukosekana mahali fulani fulani katika jamii hasa wakati wa uchaguzi.
1.3 Tahadhari na Himizo
Kutokana na viashiria hivyo hapo juu, tunapoelekea Uchaguzi wa Vitongoji, Mitaa na Vijiji mwaka huu 2004 na Uchaguzi Mkuu 2005, wapiga kura wanatahadharishwa sana na kuonywa na dhamira ya Mungu, kuchagua viongozi wenye sifa zinazostahili na hasa zilizojengwa katika msingi wa uadilifu. Aidha wadau wote wa uchaguzi ikiwemo Serikali, Wasimamizi wa Uchaguzi, Viongozi wa Siasa na wafuasi wao, Viongozi wa Dini na wengineo wanao wajibu wa kuhakikisha kuwa Uchaguzi wa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani unakuwa huru, wa haki na wa amani.
Sisi Viongozi wa Dini tunapaswa kutambua jitihada za kukuza demokrasia na hivyo kuwa makini na jasiri kuhimiza watu wafuate haki na dhamiri safi. Sisi wenyewe pia tuonywe na dhamiri zetu dhidi ya kujiingiza katika kampeni za uchaguzi zisizofaa.
Ili kulinusuru Taifa letu lisijiingize katika utawala mbovu na usio wa kiadilifu lazima tukubali kwamba wajibu wa kuandaa na kuisafisha jamii ni wetu sote tukizingatia kuwa uongozi bora na mamlaka yote hutoka kwa Mungu.
2.0 WAJIBU WA PAMOJA WA KUJENGA DHAMIRI SAFI NA KUIANDAA JAMII KWA AJILI YA UCHAGUZI
2.1 Rushwa kwa Ujumla
"Nawe usipokee rushwa; kwani hiyo rushwa huwapofua macho o hao waonao, na kuyapotoa maneno ya wenye haki (Kutoka 23:8)
Rushwa ni matokeo mabaya ya mmomonyoko wa maadili katika jamii. Hivi sasa hapa nchini Tanzania, rushwa inaendelea kuonekana kukubalika kama jambo la kawaida kati ya watu na katika shughuli zao za kila siku. Rushwa kwa tafsiri nyepesi ni malipo/zawadi isiyo halali anayodai na kupokea au kutoa mtu kama sharti au njia ya kumshawishi atoe au apate huduma. Kukithiri kwa rushwa katika jamii kumeifanya hata ipewe majina mengi yanayojaribu kuficha uovu huu. Wengine huita soda, asante, chai, wino, kuvaa shati la mikono mirefu, kitu kidogo, bahasha, mshiko, posho, takrima na mengineyo.
Sote tunajua kuwa rushwa ni kansa inayoharibu na kukwamisha jitihada za maendeleo na inajenga kasumba ya kutaka utajiri wa haraka haraka bila kufanya kazi kwa bidii na uaminifu.
Viongozi wa dini tumekuwa tukikemea rushwa mahali popote tunapopata nafasi na tunapoona inafaa ikiwemo Makanisani na kwenye mikutano mbali mbali. Vile vile tumetoa matamko ya kukemea rushwa. Matamko haya ni kama lile la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) la Bagamoyo 1994, lile la Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) la 1995, Barua ya Kichungaji ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ya 1995 na Barua ya Kichungaji ya Maaskofu Katoliki wa Metropolitan ya Dar es Salaam ya 2001.
Tunarudia na kusisitiza kuwa rushwa ni dhambi ya dhuluma inayokataa fadhila ya mapendo na usawa na hivyo kukosa kutenda haki kinyume cha maagizo ya Mwenyezi Mungu yasemayo:
"Watendeeni binadamu wenzenu yale mnayotaka kutendewa nao" (Mathayo 7:12)
Watu wanataka kutendewa sawa na haki, pia wanataka kuishi kwa amani na kujaliana ili waweze kujipatia maendeleo kwa faida ya ustawi wa wote.
Kutokana na hali mbaya ya mmomonyoko wa maadili na kansa ya rushwa katika jamii yetu, tunaona kwamba wajibu wa mafundisho ya dini ni kuchangia katika jukumu la kujenga dhamiri safi za watu katika kukubali wajibu wa kinabii kwa kukemea maovu na kupambana kwa dhati na viini vya kansa ya rushwa.
2.2 Rushwa Wakati wa Uchaguzi
Tanzania imeshafanya uchaguzi mara mbili tangu irudie mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Katika kampeni za uchaguzi suala la kudhibiti rushwa limekuwa likizungumzwa na kukaziwa. Hata hivyo rushwa imeendelea kuwepo wakati na baada ya uchaguzi.
Tunapoelekea uchaguzi ujao wa 2004 na wa 2005, wapiga kura tunatahadharishwa sana na kuonywa na dhamira ya Mungu kuchagua viongozi wenye sifa zinazostahili na hasa zilizojengwa katika msingi wa uadilifu. Tunataharishwa kama ifuatavyo;
"Kisha badala yake atasimama mtu mmoja astahililiye kudharauliwa ambaye hawakumpa heshima ya ufalme, naye atakuja wakati wa amani, naye ataupata ufalme kwa kujipendekeza... naye ataziteka nyara ngome zenye nguvu kwa msaada wa mungu mgeni; na yeye atakayemkubali atamwongeza kwa utukufu; naye atawapa kumiliki wengi; naye ataigawa nchi kwa rushwa" (Danieli 11:39).
Kuna uwezekano mkubwa kuwa vitendo vya rushwa vikawepo kwa hali ya kutisha, kwani mpaka sasa kuna manung'uniko kuwa katika baadhi ya chaguzi zilizofanyika ndani ya baadhi ya vyama vya siasa, kumekuwepo na dalili na vitendo vilivyoashiria rushwa kushamiri katika chaguzi hizo. Kwa hiyo basi, kuna uwezekano katika chaguzi zijazo wa kujipenyeza viongozi ambao watajaribu kuingia madarakani kwa njia ya rushwa.
Hivyo basi, vyama vya siasa na wagombea wao wanaotoa rushwa kwa wapiga kura ambao wengi ni maskini, wanaonywa na unabii wa Mungu;
"Lisikieni hili, ninyi mnaopenda kuwameza wahitaji, na kuwakomesha maskini wa nchi mkisema:... tupate kuwanunua maskini kwa fedha na wahitaji kwa jozi za viatu ... Bwana ameapa kwa fahari ya Yakobo akisema; hakika sitazisahau kamwe kazi zao hata mojawapo" (Amosi 8:4-7).
2.3 Uongozi Bora
Neno la Mungu linatufundisha kwamba, mcha Mungu;
`Ni yeye aendaye kwa haki, anenaye maneno ya adili; ni yeye anayedharau faida ipatikanayo kwa dhuluma; akung'utaye mikono yake asipokee rushwa; azibaye masikio yake asisikie habari za damu; afumbaye macho yake yasitazame uovu" (lsaya 33:15).
Umuhimu wa uongozi katika jamii hauna mjadala. Ni wazi kuwa uongozi ni kitu cha lazima katika jamii. Swali kubwa ni kwamba, ni kiongozi wa namna gani tunayemhitaji? Jibu litakuwa ni yule mwenye sifa tarajiwa. Baadhi ya sifa hizo ni kama zilivyoainishwa na Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania 1995 kama ifuatavyo;
• Awe mcha Mungu, maana yake awe mtu anayemkiri na kumheshimu Mungu kulingana na taratibu sahihi za dini yake.
• Awe mtu mwenye kujali na kustahi watu.
• Awe mpenda haki na awe mwadilifu (Kutoka 18:21).
• Awe mkweli kwa maneno na matendo.
• Awe mpenda amani na utulivu.
• Awe mwaminifu na mwajibikaji.
• Awe mwenye uwezo wa kuongoza na upeo mpana kiakili.
• Awe mwenye sifa njema.
• Awe na moyo wa uzalendo.
• Aijue, aiheshimu na kuitetea Katiba ya Taifa letu.
• Apende kushirikiana na wote bila kujali dini, kabila,
jinsia na rangi.
• Awe shujaa na shupavu kutetea masuala ya msingi ya
Taifa letu.
Hivyo basi iii kuhakikisha kuwa matokeo ya uchaguzi ujao yanatupatia viongozi wanaofaa, Makanisa yanavishauri vyama vya siasa kuwa makini katika kuchagua wagombea wenye sifa zinazotakiwa. Viongozi kama hao watasaidia kuleta haki, usawa, heshima na maendeleo. Viongozi wanaofaa kwenye chama tawala na wale wa upinzani wenye nguvu watasaidia kuleta na kuhimiza maendeleo ya watu na kupiga vita rushwa.
Tukumbuke kuwa viongozi wema na waadilifu hulinda na kutetea haki na ustawi wa watu wote na hufanya hivyo kwa gharama kubwa ya upendo na kuokoa kundi lake na siyo kuliangamiza kundi hilo (Yohana 10: 7-16).
Hivyo basi, tunahimiza kuwa viongozi wapatikane kwa njia ya haki na sio kwa njia ya udanganyifu. Vivyo hivyo, ieleweke waziwazi kuwa, kuzembea katika kuchagua viongozi wanaofaa katika ngazi yeyote He ni kujitafutia maafa makubwa katika nchi baada ya uchaguzi.
Tunahitaji kiongozi ambaye kwanza ni mcha Mungu, kiongozi atakayepatikana kwa utaratibu wa haki, kiongozi asiye na makuu, mpenda watu, asiye na tamaa ya kujilimbikizia mali, msemakweli, asiyeogopa kutoa maamuzi, msikivu, mchapakazi na muadilifu. Tujikumbushe tahadhari iliyotolewa kwenye Tamko la Bagamoyo la 1994;
"Wenye dhamana ya uongozi wametumia nafasi zao kufuja raslimali za Taifa, kuzikanyaga haki za wananchi wanyonge na kuzigeuza kuwa ngazi za kuelekea katika kilele cha utajiri wao. "
2.4 Uchaguzi Huru na wa Haki
Kuna umuhimu kwa Serikali na Chama Tawala kujenga mazingira ya kuviwezesha Vyama vyote vya Siasa na Kijamii kushiriki kikamilifu na kwa usawa, uwazi na haki katika mchakato au hatua zote za uchaguzi kuanzia:
• Kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.
• Kuteua wagombea ndani ya vyama vya siasa
• Kufanya mikutano ya kampeni ya uchaguzi
• Kushiriki mikutano ya kampeni za uchaguzi
• Kupiga kura
• Kuhesabu kura
• Kutangaza matokeo.
Uchaguzi ukiwa huru, wa haki na wa wazi, watu wataheshimu na kukubali matokeo yake na manung'uniko wakati na baada ya uchaguzi yatapungua.
Kwa hali halisi ya Tanzania Visiwani, Sisi Viongozi wa Dini tunahimiza kuwa haki za msingi za raia ziheshimiwe. Raia wote wa Tanzania watendewe haki sawa. Kama Watanzania wote wana haki ya kupiga kura Bara, na Visiwani, pasiwepo ubaguzi au vitisho juu ya haki ya raia kupiga kura au kuchaguliwa kuwa viongozi. Tunalohitaji ni haki, amani, kuheshimiana na kushirikiana katika kuendeleza nchi yetu.
2.5 Uwazi na Usawa katika Chaguzi ndani ya Vyama vya Siasa
Matukio mbali mbali yameonyesha kuwa baadhi ya viongozi wa siasa wamegeuza vyama wanavyoviongoza kuwa mali yao na haki yao kuviongoza maishani. Wanahakikisha kuwa mizengwe mbali mbali inatumika kuwabakiza katika uongozi.
Hali hii inakinyima chama chenyewe fursa ya kupata viongozi wengine ambao pengine wangekuwa bora zaidi na wenye upeo mkubwa wa kuleta maendeleo kwa wananchi. Pia inawanyima wanachama haki yao ya kikatiba ya kugombea nafasi za uongozi katika vyama vyao na kuweza kushinda. Uwazi, haki na usawa katika hatua ya kuwapata wagombea wa uongozi unakosekana katika baadhi ya vyama vya siasa. Usiri umetawala katika zoezi hilo.
Vyama vya siasa havina budi kuweka taratibu nzuri ambazo haziruhusu kupatikana kwa viongozi wabovu, wasio na uadilifu na wenye tamaa ya kupata utajiri wa haraka kwa kutumia nafasi zao au raslimali za umma.
2.6 Upinzani wenye Nguvu
Kwa mtazamo wetu tunaona kwamba upinzani wenye nguvu una faida kwa wananchi na hata kwa chama tawala na serikali iliyopo madarakani. Upinzani wenye nguvu imara ni kioo cha chama tawala na serikali yake. Pia upinzani wenye nguvu imara utasaidia kukemea rushwa katika uchaguzi na sekta nyingine na kuendelea kuhimiza maendeleo ya watu hata baada ya uchaguzi.
2.7 Wanawake, Watu wenye Ulemavu na Vijana
Sisi Makanisa tunatoa wito kwa vyama vya siasa, asasi za kiraia, viongozi wa dini na serikali kuwahamasisha wanawake, watu wenye ulemavu na vijana kujitokeza kwa wingi katika;
• Kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.
• Kugombea nafasi za uongozi.
• Kushiriki katika mikutano ya kampeni.
• Kupiga kura.
Kwa mfano ili kufikia lengo la SADC la wanawake kuingia katika nafasi mbali mbali za uongozi kwa asilimia 30 ifikapo 2005, juhudi za makusudi za serikali, vyama vya siasa, makanisa na wadau wengine zinahitajika.
2.8 Vyombo vya Habari katika Uchaguzi
Vyombo vya habari vina nafasi kubwa na muhimu katika kuelimisha jamii na kufanikisha uchaguzi endapo vitazingatia kanuni za kuwa huru na kutopendelea upande wowote ule. Hivyo basi, sisi Viongozi wa Makanisa tunavihimiza vyombo vya habari kuvipa vyama vyote na wagombea wao nafasi sawa na ya kutosha katika kuvitumia vyombo vya habari. Ni muhimu kuzingatia maadili ya mawasiliano katika kuelimisha juu ya uchaguzi, kutanya utafiti na kutoa habari sahihi na za kujenga; kabla, wakati na hata baada ya uchaguzi.
2.9 Raslimali
Ili kuwepo na usawa katika mchakato mzima wa uchaguzi ipo haja ya kuvipa vyama vyote vya siasa fursa sawa na kuviwezesha kiuchumi.
2.10 Tume ya Taifa ya Uchaguzi
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ina dhamana ya kusimamia Uchaguzi Mkuu hapa nchini. Ni wajibu wa Tume kuhakikisha kuwa inajenga imani kwa wananchi na kwa vyama vya siasa kuwa ni Tume iliyo huru, adilifu na makini katika kusimamia mchakato mzima wa shughuli za uchaguzi. Tunashauri kupanuliwa wigo wa wajumbe au ushiriki katika Tume ya Uchaguzi ili kupunguza manung'uniko.
2.11 Sheria ya Uchaguzi
Katiba ya nchi yetu inaheshimu uhuru na haki za msingi za binadamu. Hivyo sheria ya uchaguzi ihakikishe kuwa inajenga mazingira mazuri ya kutatua migogoro inayojitokeza katika mchakato mzima wa uchaguzi. Kwa kufanya vile itaweza kuweka mazingira mazuri ya kuwa na uchaguzi ulio huru, wa haki na wa amani.
2.12 Serikali
Sisi Viongozi wa Dini tunaishauri Serikali iendelee kuboresha taratibu za uchaguzi iii kupunguza maeneo yenye malumbano ili viongozi watakaopatikana wawe na uhalali usiobishaniwa.
2.13 Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
Taratibu za kuandikisha wapiga kura zimebadilika kutokana na uamuzi wa kuanzishwa kwa daftari la kudumu la wapiga kura. Kwa kuwa daftari la kudumu la wapiga kura ni utaratibu mpya kwa Watanzania, uzoefu wa matumizi ya daftari kwa nchi nyingine (kama vile Malawi) umeonyesha udhaifu wa matumizi yake hasa kwa mara ya kwanza. Hivyo sisi Viongozi wa Makanisa ya CCT na TEC tunasisitiza mambo yafuatayo ili kufanikisha uandikishaji wa wapiga kura kwenye daftari hilo:
• Kuwepo na matayarisho ya mapema iii kusiwepo na utata wa uandikishaji wa wapiga kura.
• Wadau wengi washiriki katika kuhamasisha wananchi kujiandikisha kwenye daftari hilo.
• Kuwepo na muda wa kutosha wa wapiga kura kujiandikisha na kukagua orodha ya waliojiandikisha katika daftari la awali (Provisional Voters Register).
• Kila mwananchi mwenye sifa za kupiga kura ahakikishe amejiandikisha. Ni daftari hili pekee litakalothibitisha upigaji kura wake kabla na baada ya kupiga kura.
2.14 Uchaguzi wa Amani na Utulivu
Udumishaji wa amani na utulivu ni jambo muhimu katika uchaguzi. Vurugu, mapambano na maonevu huwanyima wapiga kura haki yao ya kushiriki kikamilifu katika hatua zote za uchaguzi.
Chanzo cha ukosefu wa amani ni rushwa, kukosekana kwa haki, heshima na hali ya kutaka kushinda uchaguzi kwa wagombea na wafuasi wao hata kama wameshindwa kihalali. Makanisa yanatoa wito kwa wagombea na wafuasi wao wajenge utamaduni wa kidemokrasia wa kushindana bila kupigana, kuheshimu na kukubali matokeo ya uchaguzi. Ikumbukwe kuwa kila raja ana haki ya kikatiba ya kupiga kura na kugombea nafasi yeyote He ya uongozi kama ana sifa na uwezo unaostahili.
3.0 HITIMISHO
Kipimo cha ukomavu wa siasa wa Watanzania ni ushiriki wetu katika chaguzi mbalimbali ukiwemo Uchaguzi wa Viongozi wa Vitongoji, Mitaa na Vijiji wa mwaka 2004 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 wa Madiwani, Wabunge na Rais. Hii itaonyesha kuwa Watanzania tumeiva na kukomaa katika demokrasia ya vyama vingi.
Sisi viongozi wa CCT na TEC tutakuwa makini na jasiri katika kuhimiza watu wafuate haki na dhamiri safi huku na sisi wenyewe tukionywa na dhamiri yetu dhidi ya kujiingiza katika kampeni zisizofaa. Tunawahimiza Watanzania basi kutokubali kurubuniwa na kunyang'anywa haki zao za msingi. Ikumbukwe kwamba, anayethubutu kununua haki ya mpiga kura, hawezi kutetea haki za raia bila kutegemea kujilipa kwa gharama anazoziingia kwa sasa.
Ili kulin uru Taifa letu kutotumbukia katika utawala mbovu na usio wa kiadilifu, lazima tukubali kwamba wajibu wa kuisafisha na kuisaidia jamii ni wetu sote, tukizingatia kuwa uongozi na mamlaka yote hutoka kwa Mungu.
Mwisho, sisi Viongozi wa TEC na CCT tunahimiza sala na maombi. Ni kwa njia ya sala na maombi na mwangaza wa Roho wa Bwana, tutaweza kufanikisha zoezi la uchaguzi.
Tunaamini kwamba kwa nguvu za Mungu, nchi yetu itazidi kuneemeka na kusonga mbele. Tusali, tuwajibike, tutafute haki na kuitenda. Tuendelee kuliombea Taifa letu ili lizidi kuwa na amani, umoja, upendo, kuheshimiana na maendeleo yanayowalenga Watanzania wote.
MUNGU IBARIKI TANZANIA