Text Size

Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Kuhusu Hali ya Sasa ya Nchi yetu

Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Kuhusu Hali ya Sasa ya Nchi yetu
23 Februari 2001

Ndugu Watanzania na Watu Wote Wenye Mapenzi Mema,
Sisi Maaskofu tuliokutana katika mkutano wetu wa kawaida wa Kamati Tendaji kuanzia tarehe 21-23 Februari, 2001 Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Kurasini, Dar es Salaam, tunatoa masikitiko yetu makubwa kwa yale ambayo yametokea tarehe 26 na 27 Januari mwaka 2001. Watu wasiopungua ishirini na watatu walipoteza maisha yao na wengi kujeruhiwa kutokana na ghasia zilizofuatia maandamano ya kisiasa yaliyokuwa yamezuiliwa na Serikali. Vile vile tunatoa pole kwa wafiwa, walioumia, wanaoendelea kuhangaika na waliogubikwa na giza la simanzi. Aidha, tunaunga mkono tamko lililotolewa na viongozi wa dini tarehe 8 Februari, 2001 kuhusu hali ya siasa nchini Tanzania.
Tuonavyo sisi, tukio hili limesababishwa na mambo mbalimbali ambayo ni pamoja na hisia za kihistoria, kukosekana kwa mazungumzo ya wale wote waliohusika, kutoaminiana, k-utokubali kuwa wote ni watu wa nchi moja, kughiribiwa kwa urahisi kutokana na watu kutojua kwa undani mambo yanavyokwenda na umaskini.
Sababu nyingine ni kuwa Watanzania wengi hawajauelewa barabara mwenendo wa demokrasia ya vyama vingi. Hali hii inasababisha baadhi ya watu kuona kuwa kutokubaliana au kuhitilafiana katika jambo fulani la kisiasa ni uasi au uadui. Kwa hiyo sisi Maaskofu:
• Tunatoa wito kwa watu wote wanaohusika na wale wenye mapenzi mema na nchi yetu kutafuta mbinu na namna ya kurejesha hali ya maelewano. Tunasisitiza rai ya viongozi wa dini kwa serikali na viongozi wa vyama vya siasa kutumia njia ya kukaa na kufanya mazungumzo kwa pamoja mara kwa mara kwa lengo la kumaliza tofauti zao. Katika kutafuta maelewano, makundi mbalimbali ya jamii yahusishwe kwani yana haki na wajibu huo katika jamii. Swala la kujenga nchi yetu ya Tanzania kwa utulivu na amani linawahusu wananchi wote.
• Tunataka ukweli utafutwe na mambo yote yawekwe bayana. Wale wote au yeyote yule anayetaka au kusababisha machafuko kutoelewana, awajibishwe kwa mujibu wa sheria za nchi.
• Tunaomba itengenezwe mipango yenye mikakati ya kweli na thabiti ya kufuta umaskini na kuongeza nafasi za kazi kwa vijana.
• Tunaomba viongozi wa dini, serikali na makundi mbalimbali kuweka juhudi za dhati za kuunda Taifa moja, na kujenga uzalendo, mshikamano na upendo.
• Tunaomba elimu ya uraia iimarishwe na ipewe msukumo mpya kulingana na ukweli juu ya matatizo yetu. Hii itaepusha kuwachanganya na kuwachochea watu. La sivyo, maoni ya juu juu kuhusu matatizo yetu yanaweza kuwa kama kumwaga mafuta ya petroli katika moto.Tunawataka viongozi wawe karibu na watu wakati wa raha na dhiki.
• Tunawaomba watu wasiongozwe na jazba bali busara itumike kwa wakati wote
wanaposhughulikia masuala ambayo ni ya kisiasa na yale ambayo yanaweza kuhatarisha amani.
• Tunaomba vyombo vya dola vielimishwe vizuri na kufundishwa mbinu za kisasa za
kushughulikia ghasia na machafuko wakizingatia utu na uungwana wa raia.
• Tunatoa wito kwa waamini wa madhehebu na dini zote kufunga na kusali kwa ajili ya amani na
utulivu na tuwe na huruma ya kuwasaidia wale wote walio na shida.
• Tunawaomba watu na viongozi wote kusamehe na kusahau yale yote yaliyotokea na kuanza
kulijenga Taifa letu pamoja ambalo limepata doa kubwa.
"Heri wapatanishi maana hao wataitwa wana wa Mungu" Mt. 5:9.
Mungu Ibariki Tanzania.
Tamko hili limetolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania tarehe 23 Februari, 2001.
+Severine NiweMugizi