Text Size

Imani na Utamadunisho

Imani na Utamadunisho
Ujumbe wa kwaresima 1994
6 Januari 1994

DIBAJI
Ndugu wapendwa katika Kristu,
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kupitia Idara yake ya Kichungaji linawapelekeeeni barua hii ili kujiunga nanyi nyote katika kuadhimisha Kwaresima na Pasaka ya mwaka 1994.
Imekuwa ni desturi yetu kuchagua ujumbe maalum kila Kwaresima kwa lengo la kuwapatieni msisitizo wa Sala, Mahubiri na Tafakari juu ya Fumbo fulani la Imani yetu. Katika kikao cha Mkutano Mkuu wa Maaskofu Julai 1993, Maaskofu waliamua kuwa ujumbe wa Kwaresima mwaka 1994 uwe IMANI NA UTAMADUNISHO. Dhamira hii ina umaana wa kipekee mwaka huu kwa sababu ni mojawapo ya mada kuu zitakazojadiliwa katika Sinodi ya Maaskofu kuhusu Afrika, itakayofanyika mwezi Aprili mwaka huu, huko Roma.
Ni dhahiri kuwa Dhamira hii itaunganisha Kwaresima na Fumbo la Pasaka ya mwaka huu, pamoja na Sinodi itakayofunguliwa mara baada ya Pasaka. Sisi tunaona umuhimu wa kuunganisha matukio haya ya Imani yetu. Tunawaomba basi, Sala, Sadaka, Matendo ya Upendo, na yote tutakayotolea wakati wa Kwaresima, viimarishe azma ya Kanisa la Tanzania katika kushiriki na kufanikisha uenezaji wa Injili hapa Tanzania na pote Afrika kama itakavyoamuliwa na Sinodi ijayo. Tunawatakieni Kwaresima njema.
+Amedeus Msarikie
MWENYEKITI
IDARA YA KICHUNGAJI
UTANGULIZI
"Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema, amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao; Na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa
Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa" (Lk 4:18-19).
Kwa maneno hayo Bwana wetu Yesu Kristu alizindua rasmi kazi yake ya kuukomboa ulimwengu. Alionyesha wazi tangu mwanzo wa kazi yake kwamba alitumwa kujishughulisha hasa na fukara wasio na vitegemezo; watu walioelemewa na mizigo katika maisha yao; wale wanaonyimwa haki zao; kwa neno moja, watu wenye matatizo. Kwa msukumo pekee wa Roho Mtakatifu aliwaendea wale waliokuwa hoi bila kuwasahau wale waliokuwa nafuu kidogo.
Pindi la Kwaresima ni wakati ambapo kila mwumini mkristu anaalikwa kufuata nyayo za Bwana kwa juhudi zaidi katika kuwafikiria wahitaji wa aina mbalimbali. Barua hii ya Kwaresima inatualika tena kwenye vita vya kiroho vya kujiandaa kwa Fumbo la Pasaka kwa kuzingatia mazoezi ya kusali, kufanya kitubio, kujinyima na kufanya matendo ya huruma kwa wenzetu.
Wazo Kuu la Kwaresima ya mwaka huu ni mwaliko wa kuishi Imani yetu kikamilifu katika mazingira na utamaduni wa Mtanzania leo, yaani Mkristu kuyakabili kwa Imani mazingira, matukio na fikra za ulimwengu tunamoishi hivi leo. Kwa maneno mengine ni kupambanisha ukristu na utamaduni wetu. Kazi hii ni changamoto inayohitaji nia njema na juhudi ya kila mmoja wetu.
Katika barua hii fupi tutaeleza maana ya Imani kwa Jumla, Vipengele Halisi vya Imani ya Kikristu; Kupokea Imani Hii; Imani na Utamadunisho, na mwisho Tamati.
1. MAANA YA IMANI KWA JUMLA
1.Katika lugha ya kawaida watu husema: "Nina imani na fulani" au "Sina imani na mtu huyu au na jambo hili" n.k. Maana yake ni kwamba hawaamini anayosema huyu kwa sababu maneno yake hayana ukweli ndani yake. Kuwa na imani au kutokuwa na imani na kitu fulani daima hutegemea kuweko au kutokuweko ukweli. Akili ya binadamu imejaliwa uwezo wa kung'amua ukweli katika vitu na kukubali ukweli huu. Akili isipoona ukweli, angalau kiasi fulani, inakataa kuamini kwa vile hakuna ukweli.
Watu hutambua mara hali isiyo na ukweli, na hivyo wanakataa kuipa imani yao. Kwa hiyo nguvu ya ukweli ndiyo msingi thabiti wa imani yoyote ile.
2. Katika uwanja wa Dini misingi inayotegemeza imani katika dini hizo ni kweli zinaaminiwa zimetoka kwa Mungu mwenyewe. Neno hili "Dini" linafahamika kuhusisha binadamu na Mwenyezi Mungu. Mungu kwa upande wake amemfunulia mwanadamu kweli za kinabii ambazo zinagusa undani wa dhamiri ya mwanadamu. Naye mwanadamu anazikubali kweli hizo kama tegemezi la maisha yake. Kwa mfano, kwa kawaida tunaamini kuwa kuna Mungu aliyeumba vitu vyote, ndiye anautawala ulimwengu wote, n.k. Kweli zilizo msingi wa maisha ya mwanadamu zianaaminika kwa sababu tunaamini zimetoka kwa Mungu, na hivyo haziwezi kuwa ni uwongo. Kwa hiyo basi msingi wa Imani katika dini ni Mungu ambaye hadanganyi wala hadanganyiki.
3. Kuwa na imani ni muhimu sana kwa mwanadamu. Maisha yetu kama wanadamu hayawezi kwenda bila kuwa na imani kwa watu na vitu fulani fulani, kwani Imani ni kama mwamba unaotegemeza maisha ya mtu. Kwa mfano, kutokana na imani watoto wanawategemea wazazi wao; wanafunzi wanawategemea walimu wao; abiria hujisikia salama kwa kuwaamini madereva, walaji huwaamini wapishi n.k. Pasipokuwa na imani ni vigumu sana kuishi maisha yanayomstahili mwanadamu.
II. IMANI YA KIKRISTU
Asili ya Ukristu
4. Imani ya Kikristu imetokana na ufunuo wa Mungu kumpeleka
mwanaye ulimwenguni ili awakomboe wanadamu.
"Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akampeleka mwanawe wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele (Yoh.3:16).
Mungu aliupenda sana ulimwengu, ndiyo sababu akamtoa mwanawe wa pekee. Lengo ni ili kila amwaminiye apate wokovu na kujaliwa uzima wa milele. Aidha, huyu mwana ndiye uzima wenyewe; tena ni njia ya kufikia huo uzima.
"Kondoo wangu huisikia sauti yangu; mimi nawajua, nao hunifuata. Mimi nawapa uzima wa milele; na hawatapotea milele, wala hakuna mtu atakayeweza kuwatoa mikononi mwangu" (Yoh.10:27-28). "Mimi ni njia, ukweli na uzima" (Yoh.14:6).
5. Tangu mwanzo, Imani kwa Yesu Kristu imekuwa ufunguo wa kupata msamaha na wokovu. "Kwa ajili hiyo nakuambia amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi... Alimwambia yule mwanamke, Imani yako imekuokoa, enenda kwa amani" (Lk.7:47,50) Bwana Yesu alikamilisha kazi ya ukombozi kwa Mateso, Kifo na Ufufuko wake. Matendo haya makuu ya Fumbo la Pasaka ni kitovu cha Imani ya Kikristu. Kanisa linaamini haya kwa uthabiti mkubwa na kuyaadhimisha kwa shangwe kuu kila mwaka. "Kristu Alikufa, Kristu Alifufuka, Kristu Atakuja tena!"
Ujumbe halisi wa Imani ya Kikristu ni Habari Njema kwa watu wote, na hii ndiyo maana halisi ya neno INJILI. Ujumbe huu unawaalika wote wanaousikia watubu na kuamini.
"Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia, tubuni na kuiamini Injili (Mk.1:14).
6. Kabla ya kuondoka duniani Bwana wetu aliwaachia wafuasi aliokuwa amewaandaa taratibu za kuendeleza na kusimamia kazi yake. Aliwaagiza wangoje mpaka wampokee Roho Mtakatifu, halafu waende duniani kote kuhubiri ile Habari Njema.
"Enendeni mkayafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu, na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi" (Mt.28:19-20).
Kwa maagizo haya Yesu aliwaachia mitume wake kazi ya kuhubiri Imani ya Kristu, Kubatiza, na kuweka taratibu zote za usimamizi wa Kanisa lake. Anayewasikiliza hao anamsikiliza Yesu; naye amsikiaye Yesu amsikia Baba aliyemtuma.
"Anayewasikiliza ninyi ananisikiliza mimi; na anayekataa kuwapokea ninyi, anakataa kunipokea mimi. Yeyote anayekataa kunipokea, anakataa kumpokea yule aliyenituma" (Lk.10:16). Kwa utaratibu huu Imani ya Kikristu inadumishwa na kuendelezwa ulimwenguni kote.
Kanuni ya Imani
7. Mafundisho ya Imani ya Kikristu yamehifadhiwa kwa kifupi katika mihutasari au kanuni mbili zinazojulikana zaidi. Ya kwanza ni Kanuni ya Kitume ambayo husadikiwa ilianzishwa nyakati za Mitume. Kanuni hii hutumiwa katika sala na ibada za kawaida inapohitajika kutamka ungamo la imani. Kanuni ya pili inajulikana kama Kanuni ya Nicea kwa kuwa ilitokana na Mtaguso Mkuu wa Nicea 325. Kanuni hii hutumiwa wakati wa Misa Takatifu na ibada rasmi zinazohitaji ungamo la Imani. Ifuatayo ni Kanuni ya Imani ya Kitume:
"Nasadiki kwa Mungu Baba Mwenyezi, Muumba mbingu na nchi. Na kwa Yesu Kristu, mwanaye wa pekee, Bwana wetu, aliyetungwa kwa Roho Mtakatifu, akazaliwa na Bikira Maria, akateswa kwa mamlaka ya Ponsyo Pilato, akasulibiwa, akafa, akazikwa; akashukia kuzimu; akafufuka siku ya tatu katika wafu; akapaa mbinguni; amekaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi, toka huko atakuja kuwahukumu wazima na wafu. Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Kanisa Takatifu Katoliki, ushirika wa Watakatifu, maondoleo ya dhambi, ufufuko wa miili, uzima wa milele. Amina".
III. KUPOKEA IMANI
8. Imani ni paji analopewa mwumini kwa kuangaziwa na kuvutwa na Roho Mtakatifu. Mwenye kuipokea huangaziwa akilini kukubali ukweli wa kiimani na kuvutwa kuupokea kwa upendo wa Mungu. Njia ya kawaida ya kuingizwa katika imani ya Kikristu ni Ubatizo ambao ni mlango mahususi kwa mtu aliyekwisha pata akili.
Mtu anayebatizwa anaingia katika uhusiano thabiti na Yesu Kristu anayepokewa kama Mungu na Mkombozi wa wanadamu wote. Mwumini huyu anajitoa atawaliwe na Kristu katika fikira, hisia, mienendo na utendaji wa maisha yake yote.
Zaidi ya hayo, kupokea imani ya Kikristu ni pamoja na kukubali kufuata mfumo wote wa Kanisa Katoliki, yaani mafundisho yake, sakramenti zake, nidhamu yake, na mafundisho yote ya Yesu Kristu.
Maisha kamili ya Ukristu ni kuachana na maisha ya kimwili na kuzingatia maisha ya utu mpya katika Kristu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.
"Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi, juu ya mambo kama hayo hakuna sheria. Na hao walio wake Kristu Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake (Wagal.5:22-24).
9. Kupokea Ukristu ni kutambua na kuthamini utu wa binadamu na kuuheshimu inavyostahili. Hii ina maana ya kukwepa na kuacha matendo yote yanayoharibu au kudhalilisha mwanadamu, kwa mfano, kutumia binadamu kama chombo cha anasa; kumnyanyasa mwanadamu; kutoa mimba; ulevi; madawa ya kulevya; mila zinazovunja haki za binadamu, n.k.
Aidha imani ya Kikristu inamwelekeza mwanadamu kwenye matumaini ya kupata heri ya maisha yajayo. Imani inaweka mbele yetu uhakika wa mambo tunayotarajia. Maandiko matakatifu yatuambia kuwa, Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo; ni bayana ya mambo yasiyoonekana (Waebr.12:1-4).
Imani ni nguzo ya maisha ya mtu hapa duniani, kwani imani inamwezesha mtu kuyapokea magumu na majaribu ya maisha kwa ujasiri na saburi, akifuata mfano wa Yesu mwenye kuanzisha na kutimiza imani yetu. Yeye aliustahimili msalaba na sasa ameketi kuume kwa Baba katika utukufu (Waebr.12:1-4).
IV. IMANI HAI KATIKA MAISHA YA MKRISTU
10. Imani ya kweli ni ile inayojidhihirisha katika kutenda. Yafaa nini mtu akisema anayo imani lakini hana matendo? Imani isiyokuwa na matendo imekufa. Mwanadamu huhesabiwa kuwa na haki kwa matendo yake, si kwa imani peke yake. Imani iliyo hai ni ile inayoambatana na matendo. Mtume Yakobo katika waraka wake ameelezea kwa ufasaha mkubwa fundisho hili
(Yakobo 2:14-26).
Kwa hiyo wakati wa Kwaresima ni kipindi cha kudhihirisha imani yetu kwa matendo yanayotuhusu sisi wenyewe na ya huduma kwa wengine.
11. Kwanza, sisi wenyewe tutimize sheria ya Mwenyezi Mungu ya kufanya kitubio. Kufanya kitubio ni zoezi muhimu sana katika dini nyingi. Kwetu sisi wakristu tunajifunza jinsi taifa la Mungu walivyojihinisha kwa kitubio kikali kwa kufunga, kujipaka majivu na kujinyima starehe nyingi. Hata watoto hawakusamehewa zoezi hili. Basi hatuna budi kuzingatia kwa bidii yale mazoezi ambayo ni ya Kwaresima hasa. Kufuatana na mapokeo ya Kanisa tunafahamu kuwa Kwaresima ni wakati wa KUFUNGA, KUSALI, KUPOKEA SAKRAMENTI YA KITUBIO, KUWAPA MASKINI, yaani kutoa sadaka, na kusaidia wenzetu wenye shida.
12. Pili, yapo matendo kadhaa ya kuwasaidia wenzetu kimwili na kiroho:
KIMWILI:- Kulisha wenye njaa
- Kunywesha wenye kiu
- Kusaidia yatima na wajane
- Kuvisha wasio na nguo
- Kutembelea wafungwa
- Kuwaangalia wagonjwa walioachwa (ukimwi, bila jamaa)
- Kuwafariji walio na upweke (k.m. wakimbizi, wageni)
KIROHO:- Kuwashauri na kuwaombea wakosefu
- Kueneza Imani ya Kikristu
- Kuwafundisha wasio na maarifa
- Kuwatuliza wenye mashaka au uchungu
- Kuvumilia shida na masumbuko kwa saburi
- Kusamehe waliotukosea
- Kuleta amani katika mafarakano
- Kuwaombea wazima na wafu.
13. Imani na Ushuhuda
"Furahini kuhusu jambo hili ijapokuwa sasa, kwa kitambo kidogo itawabidi kuhuzunika kwa sababu ya majaribio mbalimbali mnayoteseka...... Shabaha yake ni kuthibitisha imani yenu. Hata dhahabu yenyewe, ambayo huharibika hujaribiwa kwa moto" (1 Petr. 1:6-7).
Yawezekana ikabidi kutoa ushuhuda wa imani kwa kukabiliana na magumu mbalimbali kama vile matukano, dharau, upinzani, chuki ya dini, n.k. Mitume na watakatifu wengi wamepitia hayo yote. Tujiunge nao kwa ujasiri na saburi. Mwenye imani asiionee aibu.
Tulizingatie onyo la Bwana wetu anaposema:
"Kila mtu anayekiri hadharani kwamba yeye ni wangu, mimi pia nitamkiri mbele ya Baba yangu aliye mbinguni. Lakini yeyote atakayenikana hadharani, nami nitamkana mbele ya Baba yangu aliye mbinguni" (Math.10:32-33).
Kutomwonea Bwana haya kunaweza kutuweka katika mazingira ya kuteswa, kukosa mali, kunyimwa mastahili ya kazi bila haki, kukosa mahitaji n.k.
Hata pengine ikawa lazima kufa kwa ajili ya heshima ya Ukristu wetu kuliko kuikana au kuiaibisha Dini yetu kwa kukiuka miiko yake, au kuvunja Amri za Mungu (Soma 2 Makabayo 6:18-310; pia sura 7).
V. IMANI NA UTAMADUNISHO
14. Neno "Utamadunisho" linazungumzwa sana siku hizi katika ulimwengu wa Kanisa. Sinodi ya Maaskofu kuhusu Afrika itachambua kwa undani mada hii katika kikao chake huko Roma Aprili mwaka huu. Kwa vyovyote vile kazi ya utamadunisho katika Kanisa itadumu nasi muda mrefu baada ya Sinodi. Kwa upande wetu tunaweza tu kugusia kwa kifupi misingi michache ya utamadunisho na ni vitu gani vinaweza kuhusishwa.
Tangu mwanzo wake Kanisa Katoliki limejitamadunisha na kuendelea hivyo kila lilipoendea tadamuni mpya, yaani limekubali kupokea tunu za tamaduni mbalimbali na kuziingiza katika maisha yake. Lile tukio la kuzinduliwa Kanisa siku ya Pentekoste limeonyesha wazi somo la utamadunisho. Siku ile walikusanyika mataifa mengi kutoka sehemu mbalimbali za ulimwengu, kila taifa likiwa na lugha na utamaduni wake. Wote waliwasikia mitume wakisema kwa lugha ya kila mmoja wao jinsi Roho alivyowajalia kutamka (Matendo 2:4). Hapo Roho Mtakatifu aliwawezesha mitume kuhubiri imani ile moja katika lugha mbalimbali. Jambo hili linaonyesha uwezekano wa kuwa na mseto katika Umoja na Umoja katika mseto hivyo kwamba kila lugha itumiwe kutangaza makuu ya Mungu (Matendo 2:11). Kwa hiyo, Injili tangu kuhubiriwa kwake, iliweza kupokea tunu kutoka utamaduni wowote, mradi hazikupingana na kweli za kiimani.
15. Fumbo lililo msingi thabiti wa kazi ya utamadunisho wa Injili ni Fumbo la Neno wa Mungu kujimwilisha. Yeye Neno wa Mungu alichukua hali kamili ya kibinadamu akaifanya iwe yake, pasipo kuacha kuwa Mungu. Kwa njia hii aliuinua ubinadamu wetu, papo hapo akatushirikisha umungu wake.
Kwa mithili hiyo hiyo tunu bora za utamaduni zinapoingiliana na kweli za kiinjili, tunu hizo zinasafishwa na kutakaswa zipate kuwa sehemu ya Ukristu wenyewe, na hivyo hulitajirisha Kanisa.
Katika tamaduni zetu yapo mambo chanya, yaani yenye kuweza kuboresha imani. Vilevile yapo mambo hasi, yaani yasiyoendana na imani, kwa mfano, uchawi, matambiko, ndoa zisizo halali, ushirikina n.k. Ni wazi kuwa upo ulazima wa kuchambua mila na desturi nyingine ili kuona ni zipi zinaendana na Ukristu. Ili jambo hili liweze kufanyika, Injili ipewe nafasi ya kuzipambanisha kweli zake na hekima zetu za jadi, mafunzo ya vijana, sanaa, fikra, hisia, mawazo na mienendo ya kila siku. Hatua hii iweze kukamilika ni lazima kuihubiri Injili katika uzito wake. Katika utamadunisho vipengele vingine vitasahihishwa na kukuzwa; vingine vitaachwa kuendana na thamani yake.
16. Baadhi ya nyanja zinazoweza kuhusishwa katika utamadunisho:
a. Maisha ya Jamii, kama vile kuwajibika katika ukoo, mshikamano wa kiukoo, miiko mizuri n.k.
b. Utakatifu wa maisha ya binadamu utiliwe mkazo; maisha yathaminiwe
c. Umoja, ukarimu, heshima kwa viongozi na wazee walio hai na waliokwisha fariki
d. Kupeana urithi na amana za jamii kwa njia ya mikataba inayohalalisha makubaliano, urithi wa utamaduni; ngonjera, nyimbo, mithali, hadithi. Vitu hivi vitumike katika kulea watoto na vijana.
e. Uzazi; heshima ya kupata watoto; hatua za kukua na kuwalea watoto; Ndoa; uhusiano wa vikundi mbalimbali katika jamii (wavulana, wasichana, watu wazima) kifo cha mwanajamii, matanga.
Utamaduni upewe nafasi katika matendo mengine ya Liturjia, k.m. Ndoa Takatifu, Sakramenti ya Upatanisho; Ibada ya Kupokea Watawa; namna za kusali na kuabudu; namna za kiafrika za kuonyesha heshima, na mengineyo.
TAMATI: HITIMISHO
17. HALI YA TANZANIA
Tunapoadhimisha Kwarezima ya mwaka huu tukumbuke hali ya nchi yetu. Kwa miaka mingi tumejenga utamaduni wa umoja, amani, utulivu na uelewano. Kwa sasa nchi yetu inaingia utamaduni wa mseto na kukubali tofauti. Iko hatari ya kusahau kuwa ingawa tunazo tofauti bado nchi yetu ni moja. Pamoja na kukubali tofauti zetu yabidi tuendeleze kila njia kulinda uelewano na amani.
Hivi karibuni zimeanza kujitokeza alama za mgongano na kutoelewana hata katika maeneo ya dini. Hii haitaleta maendeleo bora ya kiroho, kiuchumi au kisiasa. Daima nchi yetu inahitaji amani, umoja, masikilizano, ushirikiano hata pale tunapotambua tofauti tulizo nazo. Tujifunze kuishi na wenzetu walio tofauti na sisi (kuvumiliana).
18. Imani hai ni Imani inayounganika na matendo. Mt. Yakobo anatuambia katika waraka wake: "Waona Imani ilitenda kazi pamoja na matendo yake, na kwamba Imani ilikamilishwa kwa njia ya matendo" (Yakobo 2:22). Wakati huu wa Kwaresima twende kazini:
- Tutoe michango yote inayotupasa kiparokia, kijimbo, kitaifa. Tuchangie kwa ukarimu mahitaji ya Kanisa Takatifu. Tuwawezeshe wenye njaa wapate chakula; wasio na nguo wavalishwe; wasio na malazi wajisetiri, watoto wanaotupwa wahifadhiwe vituoni, waliopatwa na maradhi mabaya (k.m. ukimwi, malaria) watunzwe; wakimbizi wapate pa kuishi.
- Tuishi maisha makamilifu ya kikanisa yaani maisha ya sala, ya kupokea sakramenti na liturjia
- Tuishi maisha ya uadilifu wa kikristu kwa kufuata Amri za Mungu na za Kanisa. Wakati ni sasa, tusingojee kesho.
- Kila mmoja atimize wajibu na wito wake wa maisha: Baba Mkristu; Mama Mkristu, kijana Mkristu, Mtawa, Padre au Mkristu mseja.
- Tuwe tayari kuvumilia na kutimiza magumu kwa ajili ya Imani yetu.
"Tukisema kwamba hatuna dhambi tunajidanganya wenyewe, na ukweli haumo ndani yetu. Lakini tukiziungama dhambi zetu, basi Mungu ni mwaminifu na mwadilifu, naye atatusamehe dhambi zetu" (1 Yoh.1:8-9).
"Furahini kwamba mnashiriki mateso ya Kristu, ili muweze kuwa na furaha tele wakati utukufu wake utakapofunuliwa. Heri yenu ikiwa mnatukanwa kwa sababu ya jina la Kristu; jambo hilo linamaanisha kwamba Roho Mtukufu, yaani Roho wa Mungu anakaa juu yetu" (1 Petr. 4:13-14).
Hatima ya yote, tuwe na Upendo amabo ni kifungo cha mema yote. Maria Mama wa mkombozi atusaidie katika Kwaresma hii.
M W I S H O