Text Size

"MTAKUWA MASHAHIDI WANGU" (Mdo.1:8)

"MTAKUWA MASHAHIDI WANGU" (Mdo.1:8)
Walei wa Tanzania
20 Novemba 1994

UTANGULIZI
"Ni nani atakayetutenga na Upendo wa Kristo? Je! ni dhiki, au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba,
Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa,
Tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.
Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda." (Rom. 8: 35 - 37)
Ndugu Waumini Wapendwa,
Mtume Paulo aliandika maneno hayo kwa Warumi akiwa katika mazingira ya mahangaiko na mateso katika utume wake wa kutangaza Neno la Mungu. Kwake yeye Upendo wa Kristo ulikuwa ushindi wa uhakika.
Kipindi cha Kwaresima kinatuingiza katika fumbo la Pasaka wakati tunapotafakari juu ya Upendo mkuu wa Kristu ambaye aliwapenda watu wake upeo (Yoh. 13: 1).
Tukisukumwa na upendo huo wa Kristu (2 Kor. 5: 14) sisi Maaskofu wenu tunawaandikia ninyi walei wapendwa ili muimarike katika Upendo huo. Upendo huo uwasukume muwe na ujasiri katika utume wenu na uzae tunda la uadilifu na ushuhuda katika maisha yenu
Kama tulivyosema hapo juu, Mt. Paulo katika mahangaiko yake alitambua kuwa Upendo wa Kristu pekee ndiyo hakika ya ushindi wake na ndio ulimfanya awe na ujasiri katika utume. Katika ulimwengu wa leo hususan Tanzania kuna mahangaiko mengi: kwa mfano upotofu wa imani, utovu wa misingi ya maadili, kushamiri kwa kashfa za kidini, ubadhirifu na usimamizi mbaya wa mali, wasiwasi katika demokrasia ya kweli, n.k. Sisi Maaskofu tunawahimiza muwe na ujasiri ule ule wa Mt. Paulo. Toeni ushuhuda wa imani yenu, mkisukumwa na upendo wa Kristu hata ikibidi kuwa mashahidi.
Tunawahimiza waumini walei muwe mstari wa mbele katika kukabiliana na hali hiyo. Tambueni haki na wajibu wenu kama raia wa nchi hii kushiriki kikamilifu katika kujenga demokrasia ya kweli. Kutokana na ukweli huo ni kinyume kukaa pembeni na kuangalia tu, ni kukiuka wajibu wa utume mliopewa katika Sakramenti ya Ubatizo na Kipa imara. Mtaguso wa Pili wa Vatikano ukieleza msingi wa utume wa walei, unasema:
"Haki na wajibu wa Walei wa kuwa mitume unatokana na muungano wao na Kristu aliye kichwa. Wakiwa wameingizwa katika mwili wa Fumbo wa Kristu kwa njia ya ubatizo na kuimarishwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu katika Kipaimara, ni kwa njia ya Bwana mwenyewe wanatumwa kufanya kazi ya utume. Kama wamewekwa wakfu kwa ukuhani wa kifalme na taifa takatifu (1 Petro 2.4-10), hiyo ni kwa ajili ya kutolea sadaka za kiroho na wamshuhudie Kristu ulimwenguni kote.
Walei wanapewa upendo, ambao ni mtima wa utume wote na kulishwa ndani yao kwa njia ya sakramenti, na hasa Ekaristi.
Utume huo hutekelezwa kwa njia ya imani, matumaini na mapendo yaliyomiminwa ndani ya mioyo ya wanakanisa wote kwa njia ya Roho Mtakatifu, upendo ambao ndio amri kuu kupita zote zilizotolewa na Bwana kuwahimiza Wakristu wote watende kazi zote kwa utukufu wa Mungu kwa ujio wa utawala wake. Papo hapo wanakanisa hawana budi kuwashirikisha watu wote uzima wa milele, waweze kumjua Mungu mmoja aliye wa kweli na Yesu Kristu aliyemtuma (Yoh.17.3).
Wakristu wote wanao wajibu mkubwa wa kufanya watu wote duniani kote wasikie na kupokea ujumbe wa Mungu unaohusu wokovu wao.
Roho Mtakatifu hutakatifuza Taifa la Mungu kwa njia ya huduma na Sakramenti. Hata hivyo, kwa ajili ya utekelezaji wa utume, Roho Mtakatifu huwajalia waamini karama za pekee (1 Wakor. 12:7) akimgawia kila mmoja kama apendavyo (I Wakor. 12:11); kwa hiyo kila mmoja wao, na wote kwa pamoja, wakitumia neema zile walizopewa kwa ajili ya wengine, wawe mawakili waaminifu kwa zawadi hizo mbalimbali za Mungu (1 Petro 4:10), kwa ajili ya kujenga mwili wote katika upendo (Efeso 4:16). Kutokana na karama hizo, hata zile ambazo ni za kawaida kabisa, kila mwumini ana wajibu na haki ya kuzitumia karama hizo katika Kanisa na katika ulimwengu kwa manufaa ya watu na ustawi wa Kanisa. Karama hizi hazina budi kutumika katika uhuru wa Roho Mtakatifu ambaye hupuliza pale apendapo (Yoh.3:8), na papo hapo akiwa katika ushirika na ndugu zake katika Kristu, na hasa na wachungaji wote. Ni wajibu wa wachungaji kuzichunguza karama hizo ili waone iwapo ni za kweli, na iwapo zitatumika ipasavyo, siyo kwa lengo la kumsimamisha Roho, bali kwa lengo la kujaribu kila jambo na kudumisha yale yote yaliyo mema"! (1 Thes. 5:12,19,21) [Apostolicam Actuositatem No. 3).
Ushuhuda tunaozungumzia ni:
1.Kuwa na imani sahihi kama iliyofunuliwa na Kristu na inayohifadhiwa na kufafanuliwa na Kanisa Katoliki.
2.Kumwamini Kristu mwenyewe na mafundisho yake.
3.Uaminifu kwa imani hiyo
4.Kuishi na kutenda kadiri ya imani
5.Ikibidi, kuwa tayari kufa shahidi, ndiyo kilele cha ushuhuda huo.
"Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake" (Wafil. 1: 29).
HALI HALISI:
Ushuhuda katika uchumi:
Hali ya kuyumbayumba kiuchumi hapa Tanzania imesababisha ubinafsi, wizi, ujambazi, rushwa, kukoseana haki za msingi, n.k. Wengi wetu tumechangia kwa namna fulani katika kuendeleza hali hiyo. Kwa njia hiyo tumekosa kutoa ushuhuda wa kuwa mawakili waaminifu kwa yale tuliyokabidhiwa na Mungu.
Ushuhuda katika Siasa:
Nchi yetu inapita kutoka katika mfumo wa chama kimoja kuingia katika mfumo wa vyama vingi. Uchaguzi mkuu uko karibu sana.
Tunamshukuru Mungu kuwa hali ya kisiasa nchini mwetu mpaka sasa ni tulivu. Hata hivyo kuna umuhimu wa kuangalia kwa makini mapungufu kadhaa yanayoweza kujitokeza.
Kwa mfano:
-Kuzembea kujiandikisha katika kupiga kura na kupigiwa kura;
-Udanganyifu katika kupiga kura
-Kutokuwa na haki sawa ya kuteuliwa na kuchaguliwa kikatiba na
-Kampeni zisizofuata sheria za uchaguzi.
Kwa hiyo ni wajibu wa kila raia mwema kushiriki katika jitihada za kuunda serikali bora yenye majukumu ya kusimamia mwenendo wa kisiasa katika taifa letu. Kwa maelezo zaidi tazama Barua yetu ya Kichungaji "Dhamira Safi, Dira ya Taifa Letu" (uk. 24-27).
Huduma za Jamii:
Elimu:
Katika uwanja huu, elimu imezorota hapa nchini kwa sababu mbalimbali kama vile, ukosefu wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, nidhamu duni, maandalizi duni ya walimu, kushuka kwa ari ya kusoma, ongezeko la uharibifu wa shule, maslahi yasiyotosheleza ya walimu na upungufu wa fedha za kuendeshea shule.
Afya:
Kadhalika katika sekta ya afya tunaona mapungufu yafutayo; kuchelewesha mishahara ya wafanyakazi, ukosefu wa madawa muhimu, uchakavu wa majengo na vifaa vya afya, kugeuza huduma kuwa biashara, utekelezaji mbaya wa sera ya kuchangia huduma za afya, n.k.